WAPINZANI CONGO WAMJARIBU RAIS KABILA

Etienne Tshisekedi, the leader of Union for Democracy and Social Progress (UDPS) in DR Congo
Etienne Tshisekedi, kiongozi wa chama cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo


Chama kikuu cha upinzani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kimewataka wananchi kutomtambua Joseph Kabila kama rais, kikiwataka kufanya maaandamano ya amani kumpinga.

Kiongozi wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), Etienne Tshisekedi, amekiita kitendo cha Kabila kubaki madarakani kuwa ni kinyume na sheria na ni kitendo haramu na kwamba ni sawa na mapinduzi ya kijeshi.

Rais Kabila aliingia madarakani mwaka in 2001, mara baada ya kuuawa kwa baba yake. Mwaka 2006, mabadiliko ya katiba yalifanyika na kuweka ukomo wa urais kuwa vipindi viwili tu ambapo leo tarehe 20 ndio siku ya mwisho kikatiba ya kuhudumu kama rais na hivyo kumzuia kugombea kwa muhula wa tatu lakini amegoma kuachia ngazi.

Mnamo mwezi Oktoba, tume ya uchaguzi nchini humo ambayo inalaumiwa na vyama vya upinzani kuwa inashirikiana na Kabila, ilitangaza kuahirisha uchaguzi ambao ungefanyika Desemba 2016 na kuusogeza mbele mpaka Aprili 2018, na hivyo kumpa fursa bwana Kabila mwenye umri wa miaka 45 kuendelea kubaki madarakani.

Uamuzi wa tume hiyo na ule wa bwana Kabila wa kuendelea kubaki madarakani uliwakasirisha wapinzani, hasa katika mji mkuu Kinshasa, na hivyo kuitumbukiza nchi hiyo katika mzozo wa kisiasa na kuibua ghasia za mara kwa mara kwa kipindi cha miezi miwili sasa.


Mnamo mwezi Septemba yaliibuka makabiliano kati ya polisi na waandamanaji mjini Kinshasa waliokuwa wakimtaka Kabila kujiuzulu. Zaidi ya watu 50 walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Leo Tshisekedi mwenye umri wa miaka 84 aliitolea wito Jumuiya ya Kimataifa kutoendelea kushirikiana na Joseph Kabila kama Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Taarifa zinasema kuwa japokuwa serikali imepiga marufuku maandamano, waandamanaji wamekuwa wakifanya maandamano nchi nzima kwa siku kadhaa sasa na waandamanaji kadhaa wametiwa nguvuni hasa katika mji wa Goma mashariki mwa nchi hiyo.

Japokuwa Tshisekedi amewataka watu kuandamana kwa amani dhidi ya bwana Kabila, ujumbe wake wa video unaweza kuitumbukiza nchi hiyo katika ghasia zaidi kwa sababu Rais amedhamiria kukabiliana na upinzani wowote dhidi ya mamlaka yake.

Nchi hiyo iliwahi kukumbwa na matatizo mengi kwa miongo kadhaa hususan vita katika eneo la mashariki ambavyo vililipuka tangu mwaka 1998 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 5.5.

Makumi ya makundi ya waasi yamekuwa yakiendesha harakati zake katika eneo la mashariki tangu wakati huo, na jeshi la serikali likiungwa na vikosi vya Umoja wa Mataifa limekuwa likipambana na waasi hao.


Waasi hao wamekuwa wakituhumiwa kufanya mashambuli na vitendo vya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na ubakaji na kuwasajili watoto katika jeshi.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.