
KUALA LUMPUR
Waziri Mkuu wa Malaysia, Najib Razak, ameitolewa wito
serikali ya Myanmar kukomesha mara moja aina zote za dhulma za kijeshi dhidi ya
Waislamu wa jamii ya Rohingya kama inataka kuwa na uhusiano mzuri na nchi zote
za Kiislamu.
"Kama rafiki mkubwa na wa muda mrefu wa Myanmar, ninalisema
hili kutoka kwenye kina cha moyo wangu – ni muda wa kukomesha mgogoro huu [katika
mkoa wa Rakhine]," Razak aliuambia mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mambo
ya Nje wa Nchi za Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) wanaokutana kujadili suala la
Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Mkutano huo wa siku moja unafanyika mjini Kuala Lumpur na
kuhudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi zote 57 ambao ni wanachama
wa OIC.
Waziri mkuu huyo alitoa wito wa kukomesha mara moja
ukatili unaofanywa dhidi ya jamii hiyo ya Rohingya.
"Kwanza kabisa, mauaji yanatakiwa kukomeshwa;
uchomaji wa makazi unatakiwa kukomeshwa; dhulma dhidi ya wanawake na mabinti
unatakiwa kukomeshwa; unyanyasaji dhidi ya ndugu zenu, eti kwa sababu tu ni
Waislamu, unatakiwa kukomeshwa; na suala la kuwanyima haki za msingi binadamu
wenzenu linatakiwa kukomeshwa," alionya. Razak aliendelea kusema kuwa OIC
imeitaka serikali ya Myanmar kuruhusu upelekaji wa misaada ya kiutu katika
maeneo yaliyoathirika.
Alisema kuwa Malaysia itatoa msaada wa dola milioni 2.25
kwa lengo la kusaidia juhudi za kiutu na ujenzi wa miradi ya kijamii katika
mkoa wa Rakhine kama vile shule na hospitali.
"Wakati huo huo, tunaitolea wito serikali ya Myanmar
kuandaa mazingira salama na amani ya kurejea kwa wakimbizi katika makazi yao na
jamii zao kwa heshima," alisema na kuongeza kuwa kwa sasa Malaysia inawahifadhi
wakimbizi wapatao 50,000 wa jamii ya Rohingya.
Razak alisema kuwa OIC ina wasiwasi kwamba jamii hiyo
iliyodhulumiwa inaweza kuingiziwa kasumba za misimamo mikali iwapo suala hilo halitoshughulikiwa
kikamilifu.
Alisema kuwa nchi wanachama wa OIC wanatambua vizuri
kwamba makundi ya kigaidi kama vile Daesh yanaweza kuitumia hali hiyo kama
fursa kwao.
"Hilo litaitia wasiwasi jamii yote ya kimataifa, kwa
kuwa makundi ya kigaidi yanapopata makao mapya husababisha vifo na maangamizi
yanayoweza kuvuka mipaka ya nchi husika na eneo zima kwa ujumla."
Aidha, alisisitiza kuwa msimamo wa umma wa Malaysia
kuhusu mateso ya jamii ya Rohingya haumaanishi kuingilia mambo ya ndani ya Myanmar.
Hata hivyo, lisema kuwa mataifa hayo hatokaa kimya,
hususan katika hali ambayo masuala ya ndani ya nchi fulani yanaposababisha
ukosefu wa uthabiti kwa nchi nyingine.
Makundi ya watetezi wa jamii ya Rohingya yanadai kuwa
mamia ya watu wa jamii hiyo wameuawa katika operesheni za kijeshi katika mkoa
wa Rakhine kaskazini mwa nchi hiyo tangu Oktoba 9 baada ya kuuawa kwa polisi 9
kwenye mpaka wa Myanmar, huku serikali ya Myanmar ikisema ni watu 91 tu
waliouawa, yaani askari 17 na watu wengine 74 wanaodaiwa kuwa washambuliaji.
Mashirika ya kiutu yametoa wito wa kufanyika kwa
uchunguzi huru kuhusu mashambulizi hayo ya mwanzo, operesheni zinazoendelea na
visa anuai vya ubakaji na ukiukaji wa haki za kibinadamu katika mkoa wa Rakhine,
kwa sababu makundi ya kutetea haki za binadamu na waandishi wa habari
wamezuiliwa kuingia eneo hilo baada ya kuwekwa chini ya udhibiti wa kijeshi.
Tangu Oktoba, Malaysia imekuwa ikiikosea serikali na
jeshi la Myanmar kwa ukatili unaoendelea katika mkoa wa Rakhine, ikafuta mechi
mbili za soka zilizokuwa zimepangwa kufanyika nchini Myanmar mwezi huu wa
Januari na kutaka kukutana na Kansela wa Myanmar, Aung San Suu Kyi.
Mwezi Desemba mwaka jana, naibu mkurugenzi mkuu wa ofisi
ya Rais wa Myanmar alitoa jibu kuwa misingi ya Jumuiya ya Mataifa ya Kusini
Mashariki mwa Asia (ASEAN) – ambayo nchi zote mbili ni wanachama – inakataza nchi
moja kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Zaw Htay aliiambia Myanmar Times kwamba watazungumza pia
na balozi wa Malaysia kuhusu maandamano dhidi ya Myanmar na kuulizia iwapo
waziri mkuu wa Malaysia alikuwa akishiriki.
"Kama ni hivyo, tutafuatilia tukio hilo," Zaw
Htay alisema.
Mnamo mwezi Desemba, Razak aliongoza maelfu ya
waandamanaji – wakiwemo maelfu ya watu wa jamii ya Rohingya, wengi wakiwa ni
wakimbizi – kumwambia Suu Kyi – ambaye ni mshindi wa tuzo amani ya Nobel --
"kwamba sasa inatosha ".
"Nilimtaka waziri wangu wa mambo ya nje kukutana
naye mara moja ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo, lakini alilikataa mara moja,"
alisema.
"Alimwambia waziri wangu kwamba angependa kukutana
nasi kwenye masuala ya uhusiano wa Malaysia na Myanmar lakini sio suala la Rohingya.
Hii ndiyo fikra ya mtu aliyeshinda tuzo ya Amani ya Nobel."
Aidha, Razak aliituhumu serikali ya Myanmar kwa kumuonya
kuhusu uratibu wa maandamano hayo, lakini alisisitiza kuwa serikali ya Malaysia
“haina hofu ya mashinikizo hayo ya kidiplomasia".