ZUMA ATAKA WATU WASIITEMBELEE ISRAEL

South Africa president tells people to not visit Israel
Rais wa Afrika Kusini Jacob ZumaJOHANNESBURG

Rais Jacob Zuma amewataka raia wa Afrika Kusini kutoitembelea Israel isipokuwa kwa safari zinazohusiana na “kustawisha amani” katika eneo la Mashariki ya Kati.

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya kuasisiwa kwa chama chake cha African National Congress (ANC) mjini Johannesburg leo Jumapili, Zuma alisema: "Watu wa Palestina wanaendelea kupata mateso katika harakati za kudai haki yao ya kujitawala”.

Zuma ambaye pia ni kiongozi mkuu wa ANC, alisema kuwa chama chake  kiliahidi kuendeleza “mshikamano na kuunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina.”

alisema: "Hatuwashauri kutembelea Israel kwa safari zisizohusiana na ustawishaji wa amani."

Aidha, Kiongozi huyo wa Afrika Kusini alitoa wito wa kuwepo mshikamano kati ya makundi ya Kipalestina na kusema kuwa chama chake kiliunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoilaani Israel kwa sera zake za makazi ya walowezi.

Wanafunzi, wafanyabiashara na maafisa ambao walikuwa wakiitembelea Israel wamekuwa wakikosolewa kwa kitendo chao hicho.

Wananchi wengi wa Afrika Kusini, wakiwemo wanachama wa chama tawala cha ANC wamekuwa wakiiunga mkono waziwazi harakati ya Wapalestina dhidi ya ukaliaji kimabavu wa utawala wa Israel kwenye maeneo ya Wapalestina.

Waafrika Kusini wengi wanaamini kuwa kinachotokea Palestina ni sawa na kile kilichowatokea wakati wa zama za ubaguzi wa rangu uliodumu kwa miongo mingi ambao ulifikia kikomo mwaka 1994.

Aidha, Rais huyo aliitolea wito Marekani kukirejesha kisiwa cha Guantanamo Bay mikononi mwa Cuba na kuondosha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo, akisema kuwa ANC "itaendelea kusimama pamoja na wananchi wa Cuba".

Kiongozi wa zamani wa Cuba, hayati Fidel Castro, aliwahi kuunga mkono mapambano ya Waafrika Kusini dhidi ya utawala wa wazungu wachache ambao waliwanyanyasa raia weusi kwa miongo kadhaa.

Zuma alisema pia kuwa ANC itaendelea kushikamana na sera ya Umoja wa Afrika na kufanikisha azma ya Afrika yenye maendeleo na ustawi.

Rais huyo pia aliitaka jumuiya ya kimataifa kuwasaidia watu wa Syria kupata suluhisho la amani na la kudumu la mgogoro unaoikabili nchi hiyo.


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.