AUAWA KWA KUBEBA NYAMA YA NG’OMBE

Image result for cow 

Polisi nchini India imesema kuwa mtu mmoja anashikiliwa baada ya kundi la watu kumuua kijana wa Kiislamu baada ya kumshuku kuwa amebeba nyama ya ng’ombe, jambo ambalo ni kosa katika maeneo mengi ya nchi ya India yenye waumini wengi wa dini ya Kihindu.

Wahindu huwaheshimu na kuwatukuza ng’ombe, na kuchinja au kula nyama ya ng’ombe ni jambo ambalo limepigwa marufuku katika majimbo mengi nchini humo, huku baadhi ya majimbo hayo yakiweka adhabu ya kifungo cha maisha kwa mwenye kukiuka marufuku hiyo.

Junaid Khan mwenye umri wa miaka 15, siku ya Ijumaa alikuwa akisafiri kutoka New Delhi pamoja na ndugu zake watatu ndipo mapigano yalipoibuka ndani ya gari.

Wanaume kati ya 15 na 20 walichomoa visu na kuwashambulia jamaa hao huku wakitoa kauli dhidi ya Waislamu na kusisitiza kuwa mfuko mmoja waliokuwa wamebeba ulikuwa na nyama ya ng’ombe.

Wakati Khan aliuawa, ndugu yake Shakir alipata majeraha kooni, kifuani na mikononi, polisi wamesema.

Ndugu yake mwingine, Hassem, aliwaambia wanahabari kuwa kundi hilo lilipuuza ombi lao kwamba hawakuwa wamebeba nyama yoyote.

Tukio hilo ni jipya kabisa katika mfululizo wa mashambulizi yanayofanywa na waumini wa Kihindu nchini humo, ambapo kumekuwa na mlolongo wa mashambulizi dhidi ya Waislamu na watu wa jamii ya Dalit.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Waislamu wapatao 10 wameuawa katika maeneo mbalimbali nchini humo baada ya kushukiwa kula au kuuza nyama ya ng’ombe.

Wakosoaji wanasema kuwa magenge hayo yamechochewa na uchaguzi wa mwaka 2014 wa chama cha Waziri Mkuu Narendra Modi cha Bharatiya Janata chenye mrengo wa Kihindu.

Mwaka jana, Modi aliyakosoa magenge hayo na kutaka udhibiti dhidi ya makundi yanayotumia dini kama kificho cha kufanya uhalifu.


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.