QATAR YAPEWA MASHARTI YA KUONDOLEWA VIKWAZO


Emir of Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani (R) and Emir of Kuwait Sabah al-Ahmad al-Jaber Al Sabah attend a [Persian] Gulf Cooperation Council (GCC) summit on December 6, 2016, in Manama. (Photo by AFP)
Kiongozi wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani (kulia) na kiongozi wa Kuwait Sabah al-Ahmad al-Jaber Al Sabah wakihudhuria mkutano wa Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba (GCC) Desemba 6, 2016, mjini Manama.


Imeelezwa kuwa Kuwait imeipa Qatar orodha ya masharti kutoka kwa mataifa ya Ghuba yaliyoiwekea vikwazo Doha katika juhudi za kuhitimisha mzozo wa kidplomasia ulioligubika eneo la Ghuba.

Mashirika ya habari yamesema kuwa yamepata nakala ya masharti 13 kutoka kwa moja ya nchi zinazohusika na mgogoro huo. Orodha hiyo imewasilishwa na Kuwait ambayo imekuwa ikijaribu kutafuta suluhu kati ya pande mbili zinazozozana.

Kwa mujibu wa orodha hiyo, mataifa hayo yanayoongozwa na Saudi Arabia yanaitaka Qatar kukifunga kituo chake cha matangazo cha Al Jazeera chenye makao yake mjini Doha, ikate uhusiano wa kidiplomasia na Iran, ifunge kambi ya jeshi la Uturuki iliyopo nchini humo na kulipa kiwango cha pesa ambacho hakijaainishwa kama fidia.

Aidha, Doha imetakiwa kuegemea upande wa mataifa yanayounda Baraza la Ushirikiano wa Mataifa ya Ghuba kisiasa, kiuchumi na kadhalika.

Saudi Arabia na waitifaki wake pia wanaitaka Qatar kukata mahusiano yote na vuguvugu la Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood) na makundi mengine yakiwemo al-Qaeda na Daesh (Dola la Kiislamu).

Qatar imepewa siku 10 kuyatazama masharti hayo na kuyafanyia kazi.

Maafisa mjini Doha hawajatoa kauli yoyote kuhusu taarifa hiyo.

Mnamo Juni 5, Saudi Arabia na mataifa kadhaa waitifaki wake, zilikata uhusiano wa kidiplomasia na Qatar. Riyadh na washirika wake, ikiwemo Bahrain, Misri, na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), zilikata mawasiliano yote ya ardhini, baharini na angani dhidi ya Qatar kwa madai kuwa taifa hilo linafadhili ugaidi na kusababisha changamoto ya kiusalama katika ukanda mzima, madai ambayo Doha imeyakanusha vikali.

Doha imekaribisha juhudi za usuluhishi kwa lengo la kuondoa mvutano, lakini ikaweka msimamo kuwa haitaruhusu majirani zake kuwaamulia masuala mambo yake binafsi na yanayosimamia mamlaka yake kama nchi.

Qatar imesema kuwa haitaingia kwenye mazungumzo mpaka mataifa hayo ya kiarabu yaondoe kwanza vikwazo dhidi yake.

Hivi karibuni waziri wa Mambo ya Nje, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani alisema kuwa nchi yake itayategemea mataifa mengine iwapo vikwazo hivyo vitaendelea.

Hatua kali dhidi ya Qatar zimekuwa zikilaaniwa na makundi ya haki za binadamu kama vile shirika la Amnesty International, ambalo lilisema kuwa mgogoro huo wa kidiplomasia umeyaathiri maisha ya maelfu ya watu.

Kwa sasa mataifa ya Iran na Uturuki yanaipatia Qatar mahitaji ya chakula huku Uturuki ikiwa imepeleka vikosi vya askari wake kwenye kambi yake ya kijeshi iliyoko nchini humo.


Mvutano huo uliibuka mwezi jana baada ya Shirika la Habari la Qatar (QNA) kutoa kauli zilizohusihwa na kiongozi wa taifa hilo Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, zikiielezea Iran kama “Taifa la Kiislamu lenye nguvu,” kulisifu vuguvugu la Hamas la nchini Palestina na kumkosoa Rais wa Marekani Donald Trump.

Baadaye Qatar ilisema kuwa wadukuzi walikuwa wameivamia tovuti ya QNA na kuchapisha taarifa bandia, lakini kanusho hilo halikuishawishi Riyadh na waitifaki wake wa Ghuba.

Mapema Jumatano Doha ilitangaza kuwa ina ushahidi kwamba tukio hilo la udukuzi lilifanywa kutokea moja ya nchi jirani.

UTURUKI YAPINGA KUINGILIWA MAHUSIANO YAKE

Kufuatia kutolewa kwa orodha hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Fikri Isik, amesema kuwa Ankara haina mpango wa kuondosha kambi yake ya kijeshi ya nchini Qatar, akaongeza kuwa nchi hiyo inalitazama sharti lolote la kufunga kambi yake hiyo kuwa ni kuingilia mahusiano yake na Doha.

“Kambi iliyoko Qatar ni ya Uturuki lakini pia inaimarisha usalama wa Qatar na eneo zima,” Isik alisema katika mahujiano ya kituo cha NTV.

Ankara ilipelekea askari wake nchini Qatar katika hali ya kuonesha kumuunga mkono mshirika wake kufuatia kuibuka kwa mzozo huo wa kidiplomasia.

Mnamo mwaka 2014, Uturuki na Qatar zilisaini makubaliano ambayo yaliruhusu kujengwa kwa kambi ya kijeshi ya Uturuki nchini Qatar. Maafisa wanasema kuwa askari wasiopungua 3,000 wanaweza kupelekwa nchini humo kama sehemu ya programu ya Ankara ya kuongeza ushirikiano wa kijeshi na Doha.Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.