RONALDO MAHAKAMANI KWA UKWEPAJI KODI

Image result for Real Madrid star Ronaldo to appear before judge in tax evasion probe 


Nyota wa Klabu ya soka ya Real Madrid ya nchini Hispania, Cristiano Ronaldo anatarajiwa kufika mahakamani baada ya waendesha mashitaka nchini humu kumtuhumu kukwepa kodi ya kiasi cha zaidi ya Yuro milioni 14, na kumfanya kuwa katika orodha ya wachezaji waliokumbana na mkono wa mamlaka za nchi hiyo.

Msemaji wa timu ya wanasheria wa Ronaldo mwenye umri wa miaka 32, amesisitiza kuwa nyota huyo raia wa Ureno atafika mahakamani mwenyewe, huku akikataa kueleza kwa undani zaidi.

Nyota huyo ambaye jarida la Forbes limemtaja kama mwanasoka anayeingiza pesa nyingi duniani, sio wa kwanza kutuhumiwa kukwepa kodi nchini Hispania, kwani miongoni mwao wapo wanasoka kadhaa akiwemo mpinzani wake mkubwa, nyota wa Barcelona, Lionel Messi.

Mwaka jana Messi na baba yake walihukumiwa kifungo cha miezi 21 kwa kosa la kukwepa kodi yenye thamani ya Yuro milioni 4.16. Hata hivyo, mwezi Julai mwaka huu mahakama iliwabadilishia adhabu kwa kutakiwa kulipa ziada ya pesa.

Waendesha mashitaka wanamtuhumu Ronaldo kukwepa kodi ya kiasi cha Yuro milioni 14.17 (sawa na Dola milioni 17.3) na kutumia kampuni iliyoanzisha mwaka 2010 kuficha mapato aliyoyapata nchini humo kupitia haki za matangazo.

Mamlaka nchini humo zinaona kuwa alichofanya Ronaldo ni “uvunjifu wa makusudi wa wajibu wa ulipaji kodi nchini Hispania” kwa kupitia makampuni yenye makao katika Visiwa vya Virgin nchini Uingereza na mengine huko Ireland ambayo ni maarufu kwa kupuuzia suala la kodi.

RONALDO HANA WASIWASI

Aidha, mamlaka nchini humo zinasema kuwa Ronaldo aliweka wazi mapato yake nchini humo ya kiasi cha Dola milioni 11.5 pekee kati ya mwaka 2011 na 2014, ilhali kiasi halisi cha mapato yake katika kipindi hicho kilivuka Yuro milioni 43.

Vilevile, mamlaka zinamtuhumu kwamba alikataa kwa makusudi kuorodhesha mapato ya kiasi cha Yuro milioni 28.4 yenye mafungamano na haki za matangazo kati ya mwaka 2015 na 2020 kwenye kampuni moja ya Kihispania.

 Hata hivyo, Ronaldo anasisitiza tangu mwanzo kuwa hana hatia, na kwamba aliweka wazi mapato yake yote na kwa njia rasmi.

Tangu alipoelekezewa tuhuma hizo mwezi Juni mwaka jana, Ronaldo aliamua kukaa kimya ambapo muda mfupi kabla ya timu yake ya taifa kushiki michuano ya kombe la mabara nchini Urusi alisema tu kwamba hana wasiwasi kuhusu suala hilo, ambapo baada ya siku mbili akasema kuwa kukaa kimya “ni jibu zuri zaidi” dhidi ya tuhuma hizo.

Licha ya upande wa wanasheria kukaa kimya, suala hilo lilichukua nafasi kubwa katika ulimwengu wa soka, hususan baada ya kufuatiwa na mfululizo wa ripoto mbalimbali za vyombo vya habari kuhusu nia ya mchezaji huyo kutaka kuondoka katika klabu hiyo aliyojiunga nayo mwaka 2009 akitokea Manchester United.

Ripoti hizo ziliashiria kuwepo kwa uhusiano kati ya tuhuma hizo na nia yake ya kuhamia klabu tofauti katika nchi nyingine.

Hata hivyo, baadaye Ronaldo aliweka wazi na kusisitiza juu ya nia yake ya kubaki katika klabu hiyo ambayo katika msimu uliopita aliiongoza kutwaa ubingwa wa nchi hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 na kuchukua kombe la Klabu Bingwa Ulaya kwa msimu wa pili mfululizo.

Aidha, kocha wa mabingwa hao, Mfaransa Zinadine Zidane alisisitiza kuwa mchezaji wake huyo angebaki.

Kwa mujibu wa ripoti za wataalamu wa masuala ya kodi ya mapato nchini Hispania, iwapo Ronaldo atapatikana na hatia anaweza kutozwa faini ya kiasi cha Yuro milioni 28 na anaweza kupewa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu na nusu.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes, tangu Ronaldo alipoongeza mkataba wake na Real Madrid mwezi Novemba 2016 mpaka mwaka 2021, amekuwa mchezaji mwenye kuongiza mapato makubwa zaidi duniani, na katika msimu wa 2016 – 2017 alipata kiasi kipatacho Dola milioni 93.Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.