WAPINZANI VENEZUELA WATANGAZA MGOMO MPYA DHIDI YA RAIS MADURO

Photo by: Reuters
Muandamanaji akikabiliana na askari wa kutuliza ghasia wakati wa maandamano dhidi ya serikali ya Rais wa Venezuela  Nicolas Maduro mjini Caracas, Venezuela, Julai 22, 2017.


Upinzani nchini Venezuela umetangaza siku mbili za mgomo wa kitaifa dhidi ya Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro baada ya siku iliyoshuhudia ghasia na makabiliano mjini Caracas siku ya Jumamosi ambapo waandamanaji kadhaa walijeruhiwa.
Muungano wa Kidemokrasia wa vyama vya upinzani – ambao uliratibu mgomo wa saa 24 wiki hii ambao uliitikiwa na mamilioni ya watu na kulemeza sehemu kubwa ya shughuli katika taifa hilo la Amerika ya Kusini – umesema kuwa mgomo ujao utafanyika siku za Jumatano na Alhamisi.
Maandamano makubwa pia yameandaliwa kwa siku za Jumatatu na Ijumaa katika juhudi za kumlazimisha Rais Nicolas Maduro afute uchaguzi wenye utata wa bunge jipya uliopangwa kufanywa Julai 30.
Mzozo huo wa kisiasa unaokua kwa kasi katika taifa hilo unakuja baada ya zaidi ya watu 100 kupoteza maisha na maelfu wengine kujeruhiwa katika maandamano ya kuipinga serikali tangu ghasia zilipoanza mwezi Aprili.
"Wananchi wa Venezuela hawatokata tamaa, wana ujasiri, watajitokeza kuitetea demokrasia na katiba," alisema mbunge wa upinzani Simon Calzadilla kwenye mkutano na wanahabari huku akiwa amezungukwa na maafisa wengine wa muungano wa upinzani.
Wapinzani wanamtuhumu Maduro kuipeleka Venezuela kwenye udikteta na kuua uchumi. Wanataka uchaguzi huru na kuhitimishwa kwa utawala wa miongo miwili wa siasa za kisoshalisti.
Maduro mwenye umri wa miaka 54, anajitambulisha kama mbeba bendera ya siasa mrengo wa kushoto duniani dhidi ya anaowaita kuwa ni “magaidi” wa mrengo wa kulia wanaotaka kufanya mapinduzi kwa kuchochewa na Marekani na vyombo vya habari vya kimataifa.
 Upinzani unatumia mbinu ya kuingia mitaani ijulikanayo kama “saa sifuri” kwa Venezuela ili kujaribu kuzuia Bunge jipya la Katiba ambalo Maduro anataka kuliweka kwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa juma lijalo.
Wapinzani hao wamegomea uchaguzi huo wakiuita kuwa ni fedheha na badala yake wanataka kufanyike uchaguzi wa kawaida.
Bunge hilo ambalo kanuni zake zinaonekana kuipa serikali kura nyingi, ingawa ina uungaji mkono mdogo, linaweza kuandika upya katiba na kulivunja bunge la sasa linaloongozwa na upinzani.
 “TUMECHOSHWA NA UGAIDI”
 Kwenye maandamano kinzani ya wale wanaoiunga mkono serikali yaliyofanyika siku ya Jumamosi, wagombea wa Bunge la Katiba walisema kuwa hiyo ndio njia pekee ya kurejesha amani nchini Venezuela. "”Hatutowaruhusu waiharibu nchi yetu tunayoipenda," alisema Delcy Rodriguez, ambaye aliachia nafasi yake ya uwaziri wa mambo ya nje ili aweze kugombea kwenye bunge jipya.
"Sote tulioungana tunaenda kuwaambia wale wa mrengo wa kulia ‘Tumechoshwa na ugaidi’," mke wa Maduro Cilia Flores, ambaye pia anagombea nafasi kwenye bunge hilo aliuambia umati uliokusanyika kwenye maandamano hayo mjini Caracas.
Aidha, siku hiyo ya Jumamosi, idara ya upelelezi ya serikali ilimkamata Angel Zerpa, ambaye ni miongoni mwa mahakimu 13 walioapishwa na upinzani kuwa mahakimu wa mahakama kuu katika hatua ya wapinzani hao kuipinga serikali iliyopo madarakani.
Serikali imetishia kuwakamata majaji wote walioteuliwa na wapinzani na kuwafikisha kwenye mahakama za kijeshi.
 Shinikizo la kimataifa limeongezeka dhidi ya Maduro akitakiwa kufuta kura hiyo inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa juma lijalo, ikiwa ni pamoja na kitisho kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump aliyetishia kumuwekea vikwazo vya kiuchumi.
Lakini serikali haioneshi kuachana na wazo hilo, huku ikitangaza kuwa itawaweka barabarani askari wapatao 232,000 kuhakikisha kuwa Bunge la Katiba linaendelea.
 Siku ya Jumamosi, vikosi vya Walizi wa Jamhuri, vilionekana kuwarushia waandamanaji mabomu ya kutoa machozi, hatua inayochukuliwa kuwa ni ukiukaji wa kanuni za kimataifa.
 "Kumekuwepo na ukandamizaji mkubwa na dunia inapaswa kujua hali inayotukabili katika mitaa ya Venezuela," alisema kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado.Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.