TRUMP ASALIMU AMRI MBELE YA CONGRESS


Rais wa Marekani, Donald Trump
Baada ya kusita kwa muda, hatimaye Rais wa Marekani, Donald Trump ametia saini sheria inayoziwekea vikwazo nchi za Urusui, Iran na Korea ya Kaskazini hali inayoashiria kuwa amesalimu amri mbele ya mbinyo wa ndani, jambo linalotazamiwa kuzorotesha juhudi za kuboresha uhusiano na Urusi.

Trump amesaini sheria hiyo akiwa amejifungia ndani na pasipo kamera za wanahabari baada ya kushindwa katika juhudi zake za kuzuia upitishwaji au upunguzaji wa sheria hiyo.

Hali ya kusita kusaini sheria hiyo ilionekana wazi katika matamshi yake makali ambapo alisema kuwa sheria hiyo ina upungufu na “kasoro nyingi”.

SHERIA INAMZUIA RAIS KUONDOSHA VIKWAZO

Trump alisema kuwa bunge la Congress lilifanya haraka katika hatua yake ya kupitisha vikwazo hivyo ambapo alidai kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo yanakiuka katiba, ikiwa ni pamoja kuufunga uwezo wa rais kutekeleza sera zake za mambo ya nje.

Sheria hiyo, ambayo inazigusa pia Korea ya Kaskazini na Iran, inalenga sekta ya nishati ya Urusi na inaipa Washington uwezo wa kuyaadhibu makampuni yatakayoshiriki katika ujenzi wa mabomba ya mafuta ya Urusi, na inaweka vikwazo dhidi ya wanunuzi wa silaha za Urusi.

Aidha, sheria hiyo inaufunga uwezo wa rais wa kuondosha vikwazo, katika hatua inayoonesha kuwa wabunge wa Republican ambao wanalidhibiti bunge la Congress hawana imani na Trump na wanatiwa wasiwasi na matamshi ya rais wao kuhusu Rais wa Urusi, Vladmir Putin.
Vikwazo hivyo vinalenga kuiadhibu Urusi kwa madai kwamba iliingilia mchakato wa uchaguzi wa Urais wa Marekani wa mwaka 2016 ambapo bwana Trump aliibuka mshindi, na pia hatua yake ya kuimega peninsula ya Crimea.

Trump amesema kuwa “atatekeleza” baadhi ya mambo katika sheria hiyo, lakini akajizuia kusisitiza iwapo atayatekeleza yote, huku Ikulu ya nchi hiyo ikiishia kusema kuwa Trump “atazingatia kwa umakini na kwa heshima maazimio ya Congress”.

Trump alipokea muswada huo jioni ya Ijumaa lakini akawa hajaisaini mpaka Jumatano.

Hatua hiyo ya kuchelewa kusaini iliibua minong’ono kuwa Trump anaipinga sheria hiyo au anajaribu kuichelewa kwa njia moja au nyingine baada ya wajumbe wa bunge la seneti kuikubali kwa kura 98 dhidi ya kura mbili.

Kwa kusaini sheria hiyo, Trump aliepuka hatua ambayo ingechukuliwa na Congress ikiwa ni pamoja na kuipitisha kwa hali yoyote, jambo ambalo lingekuwa ni sawa na kumdunisha.

TILLERSON: UPITISHWAJI WA SHERIA HIYO KUNAWEKA MAZINGIRA MAGUMU YA KUBORESHA UHUSIANO NA MOSCOW

Mapema siku ya Jumanne, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Rex Tillerson alisema kuwa atakutana na mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov mwishoni mwa juma, lakini akatahadharisha kuwa uhusiano wa Urusi na Marekani unaweza kuzorota. Alisema kuwa hatua ya Congress kupitisha sheria ya vikwazo imefanya juhudi za kuboresha uhusiano na Moscow kuwa “ngumu zaidi”.

Moscow ambayo ilitarajia kupitishwa kwa sheria hiyo, iliiamuru Washington kupunguza wanadiplomasia wake walioko Urusi mpaka kufikia watu 455 kabla ya Septemba mosi ili iendane na ukubwa wa wanadiplomasia wa Urusi waliopo nchini Marekani.

MOSCOW YALAANI SERA “HATARI NA ZA MTAZAMO MFUPI”

Katika jibu la kwanza baada ya Trump kusaini sheria hiyo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Urusi ilikosoa vikali kile ilichokieleza kuwa ni siasa “hatari” na “za mtazamo mfupi” za Washington.
Katika taarifa yake, wizara hiyo ilisema kuwa “ni mwenendo wa siasa zisizotazam mbali na za hatari ambazo zinatishia usalama wa dunia ambao Moscow na Washington zinahusika nao kwa namna maalumu”.
 Ikiongeza kuwa: “Tumekwishatangaza kwamba hatutaacha vitendo vya kiuadui vipite bila jibu… tunasubiri kuchukua hatua nyingine kali”.

Aidha, Moscow iliitolea wito Marekani “kuachana na mambo ya kufikirika na kutambua kuwa kitisho chochote au jaribio lolote la shinikizo halitailazimisha Urusi kubadilisha sera zake au kuyatoa mhanga maslahi yake ya kitaifa”.

Pia wizara hiyo ilieleza kuwa Moscow itaendelea kufungua mikono ya ushirikiano na Marekani katika maeneo ambayo inayachukuliwa kuwa yana faida kwake na kwa usalama wa dunia, hususan katika utatuzi wa migogoro ya kieneo na kikanda.
Lakini ikasema kuwa ushirikiano hautakuwa na matunda isipokuwa pale ambapo watunga sera mjini Washington watakapoacha kuutazama ulimwengu kupitia jicho la Marekani pekee.

#Mzizima 24/ Mashirika ya habari


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.