SARKOZY MIKONONI MWA POLISI

Ex-French President Sarkozy taken into police custody

Rais wa zamani wa Ufaransa na kiongozi wa chama cha Les Republicains, Nicolas SarkozyPARIS


RAIS wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, anashikiliwa na jeshi la polisi la nchi hiyo kwa tuhuma za matumizi ya fedha chafu wakati wa kampeni yake ya kugombea urais wa nchi hiyo mwaka 2007.


Kwa mujibu wa vyombo vya habari, hivi karibuni Sarkozy alihojiwa na polisi mjini Nanterre ikiwa ni sehemu ya uchunguzi dhidi ya tuhuma za kupewa fedha na utawala wa zamani wa Libya kwa ajili ya kampeni zake za urais za mwaka 2007, gazeti la Le Monde la nchini humo limeripoti.Hii ni mara ya kwanza kwa Sarkozy kuhojiwa katika uchunguzi huo ambao ulianza miaka mitano iliyopita. Anaweza kuendelea kushikiliwa na polisi kwa muda usiozidi saa 48 na kisha anaweza kupelekwa mahakamani kwa ajili ya mashitaka rasmi.


Majaji Serge Tournaire na Aude Buresi wamekuwa wakishughulikia kadhia hiyo tangu Aprili 2013 ili kubaini iwapo kampeni hizo za Sarkozy zilihusisha fedha haramu kutoka Libya.


Mnamo Juni 2016, majaji wa Ufaransa walitoa uamuzi kuwa nyaraka zinazodai kuwa Sarkozy alipewa Yuro milioni 50 na kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi kama msaada kwa kampeni zake za uchaguzi, ni nyaraka sahihi.


Nyaraka hizo zilizofichuliwa kwa mara ya kwanza na mitandao ya habari za kiuchunguzi nchini humo mwaka 2012, zinadaiwa kuonyesha kuwa Sarkozy alifanya makubaliano na Gaddafi kwa ajili ya kufadhili kampeni zake za urais katika uchaguzi huo ambao alimshinda Segolene Royal kutoka chama cha kisoshalisti.


Mwaka 2016 gazeti la kila siku la Le Monde katika machapisho matatu mtawalia liliripoti juu ya "uwepo wa mtandao mkubwa wa kiuhalifu uliowahusisha maafisa waandamizi wenye ukaribu na Sarkozy.


" Mtandao huu, ambao ulikuwa na kazi ya kumlinda rais huyo wa zamani, unaundwa na maafisa wa polisi na mahakimu ambao waliendelea kuwa watiifu kwake, lakini pia uliwahusisha wafanyabiashara, watu wa kati, wanadiplomasia na hata waandishi wa habari," gazeti hilo liliripoti.


Mtandao huo ulidaiwa kuundwa baada ya Sarkozy kuwasili wizara ya mambo ya ndani mwaka 2002, ambapo uliimarishwa zaidi baada ya kuingia Ikulu ya Elysee mwaka 2007.


Aidha, mnamo Septemba 2016, waendesha mashitaka walishauri kuwa Sarkozy na wenzake 13 wafikishwe mahakamani kujibu mashitaka ya kutumia mamilioni ya fedha chafu kufadhili kampeni zake za urais za mwaka 2012.

Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.