WATOTO 12, DEREVA WAUAWA BAADA YA BASI LA SHULE KUGONGANA NA TRENI NCHINI INDIA


 Onlookers gather around the mangled remains of a school bus after it was hit by a train in Kushinagar district in India's Uttar Pradesh state on April 26, 2018. (AFP Photo)


Treni imegongana na basi la shule katika kivuko kimoja kaskazini mwa India leo Alhamisi na kuua watoto 12, polisi ya nchi hiyo imesema.

Afisa mwandamizi wa polisi O.P. Singh amesema dereva wa basi hilo naye amepoteza maisha.

Watoto wengine 12 wamejeruhiwa katika ajali hiyo na kupelekwa hospitali ya mji wa Kushinagar, kilometa 200 (maili 125) kusini mashariki mwa Lucknow, mji mkuu wa jimbo la Uttar Pradesh.

Wanafunzi hao walikuwa wakielekea shule wakati treni ilipoligonga basi lao.


"Waathrika wengi walifariki dunia hapohapo," afisa wa polisi katika eneo hilo,  Ramkrishna Tiwari, amesema.

Watoto hao walifariki dunia wote walikuwa na umri chini ya miaka 10, alisema. Idadi ya vifo inaweza kuongezeka kutokana na baadhi ya majeruhi kuwa katika hali mbaya.

Polisi imemtupia lawama dereva kwa ajali hiyo. "Ajali hiyo imetokea kwa sababu ya uzembe wa dereva. Alikuwa ameweka spika masikioni akisikiliza muziki na hakusimamisha basi kuangalia kama treni ilikuwa inakuja," amesema Tiwari.

Mamlaka za serikali katika jimbo hilo zimeagiza kufanyika uchunguzi huku viongozi wa India wakituma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika hao.

Wazazi na ndugu walioshtushwa na tukio hilo walikimbilia kwenye eneo la tukio na hospitalini baada ya kusikia taarifa za ajali hiyo.

Matukio ya ajali yamekuwa mengi katika vivuko vya reli nchini India. Zaidi ya watu milioni 23 hupanda treni za abiria 11,000 nchini humo kila siku.

Mamia ya vivuko hayana alama, hususan katika maeneo ya vijijini. Uhaba wa fedha hutatiza uwezo wa huduma za reli kuweka alama au walinzi katika vivuko hatari kwa wakati.

Madereva wa magari mara nyingi hujaribu kuvuka kwa kasi katika maeneo ya reli yasiyowekewa alama na hivyo kusababisha ajali.

Hii ni ajali kubwa ya pili kuwahusisha watoto wa shule katika kipindi cha chini ya wiki mbili.

Mnamo Aprili 9 watoto wasiopungua 24 na watu wazima 3 walipoteza maisha baada ya basi la shule kupata ajali katika barabara ya mlimani katika jimbo la Himachal Pradesh kaskazini mwa India.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.